Helena Ringo: Mimi ni mfano wa watu waliokeketwa
Joan Michael: Nilipokeketwa damu na usaha ilitiriria
DK.Leonard Tlatlaa: Nimekutana na mtoto njia ya uzazi imefunga
kwa ajili ya kukeketwa
Na Lucy Ngowi
“NAKUMBUKA nilipokuwa na miaka mitano nilikeketwa. Kiukweli
sitaisahau siku hiyo kutokana na maumivu niliyoyapata wakati wa kukeketwa na
kuuguza kidonda.
“Wakati naugulia maumivu ya kukeketwa, nilikuwa nikiona katika
sehemu zangu za siri damu na usaha vikitiririka, ila sijui mbele ya safari
itakuwaje, kama atakuwa na uwezo wa kupata mtoto au la,” anasema Joan Michael
(jina lisilo rasmi).
Binti huyo ambaye hivi sasa ana miaka 19 anazungumza kwa
uchungu kuelezea mila potofu zinazofanywa na kabila lake la wabarbaig.
Anasema laiti kama angechelewa kukeketwa asingekubali tena
kwani katika hali ya uhalisia ni ukatili uliopitilizwa, kwani hata kwenye
maandiko matakatifu biblia hakuna mahali inapozungumzia kuhusu kumkeketa
mwanamke bali kutahiri wanaume.
Anaiomba Serikali kuendelea kutoa elimu bila kuchoka kwa jamii
hiyo ili kuwanusuru watoto wa kike ambao bado hawajakeketwa wasipatwe mateso
ambayo alikabiliana nayo.
Si huyo tu, mfano wa binti
kama huyo ni mingi katika jamii za watu wanaokeketa ila wamekuwa
wakiogopa kuzungumza hadharani kwa kuona aibu au kuhofia kutengwa na ndugu
zake.
Kwa upande wake Mama Mchungaji wa Kanisa la Evangelistic
Assemblies of God (EAGT), Odeliana Emmanuel anasema katika kijiji cha Qandach
alikozaliwa, kata ya Endamila wilaya ya Mbulu, amekuwa akiona hali ya ukeketaji
kwa watoto wa kike.
Anasema kama mama mchungaji na mwanaharakati wa kumtetea mtoto
wa kike, amekuwa akizungumza na wale wanaowaandaa watoto kuwapeleka kwa
ngariba, kuwaelimisha na kuwafundisha athari za kukeketwa kwa mtoto wa kike.
“Nimeelimisha ubaya wa ukeketaji. Kwa sasa umepungua lakini
unaendelea kwa siri sana, hivyo wamebadili mbinu mpya ya kuwakeketa watoto
kuanzia wanapoanza kutembea,” anasema mwanaharakati huyo.
Mkuu wa Idara ya Maendeleo ya Jamii Mbulu, Halmashauri ya
Vijijini Justino Bayo anasema wilaya hiyo ina wenyeji wanaojulikana kama
wairaqw, datoga au barbaig, nyisanzo na hadzabe.
Anasema suala la ukeketaji katika wilaya hiyo sasa hivi
linapungua kwa wairaqw pamoja na wanyisanzo, lakini wa wabarbaig wanaendelea.
Lakini kama tendo hilo linafanyika katika mji huo ni
kwa siri sana kutokana na kuogopa mkono wa sheria.
Bayo anasema chanzo cha hilo ni mila na desturi za wenyeji
ambao wanaona kuwa mwanamke asipokeketwa ni kama najisi.
Naye Helena Ringo anaeleza kuwa, yuko miongoni mwa
waliokeketwa, kwani mbaya zaidi alifanyiwa kitendo hicho akiwa na miaka 19
baada ya kumaliza chuo.
“Mimi ni mfano wa watu waliokeketwa. Nilikeketwa nikiwa
nimemaliza chuo cha ualimu nikiwa na miaka 19,” anasema.
Mwanamke huyo ambaye fani yake ni mwalimu pia ni Mratibu wa
Shirika linaloshughulikia ukeketaji wanawake na wasichana (AFNET), anasema mara
nyingi mwisho wa mwaka wanawake wengi wanaandaa wasichana wao kwa ajili ya
kukeketwa.
Hivyo kama mwanaharakati amekukwa akipita shule mbalimbali na
kuwaasa wanafunzi wasikubali kukeketwa kipindi cha likizo.
Anasema amekuwa akipita katika shule za msingi na kutoa elimu
hiyo, si hivyo tu bali mara nyingi pale anapokuta watu wamekusanyika huomba
nafasi na kusema machache kuhusu ubaya wa ukeketaji.
“Nimekuwa nikiwaambia msipunguze kiungo chochote cha mtoto
katika mwili wake, endapo mtafanya hivyo akimkamata mtu yeyote anampeleka
mahakamani,” anasema mwanaharakati huyo.
Si hivyo tu, bali hata siku ya mtoto wa Afrika inayofanyika
Machi 16, huwa anatoa elimu hiyo kuhusu ukeketaji.
Anakiri kuwa tatizo hilo ni kubwa, hivyo kama wataendelea
kutoa elimu litapungua.
Anaongeza kuwa, baada ya kutolewa elimu mara kwa mara kuhusu
athari za ukeketaji tatizo linapungua isipokuwa kwa watu wa vijijini ambao
hufanya kimya kimya ili wasijulikane
wanachokifanya.
Ringo anasema chanzo cha ukeketaji ni imani iliyojengeka kuwa
wanawake wanakeketwa ili kupunguza uhuni, lakini kiuhalisia ndio waliozidi kwa
tabia hiyo mbaya.
Sababu nyingine ni kwamba wanamfanyia usafi msichana huyo kwa
sababu sehemu hiyo inaficha uchafu.
Naye Kaimu Mganga Mkuu wa Hospitali ya Wilaya Mbulu, Dk.
Leonard Tlatlaa anasema hawajapata kesi za mtu aliyezidiwa kutokana na
kukeketwa lakini kama daktari anaona kuna dalili zinazoonyesha bado kuna
ukeketaji.
Na kwamba katika eneo hilo wanakeketa watoto katika umri mdogo
kwa kuogopa mkono wa sheria.
“Kama daktari nimekutana na kesi ya mama wa mtoto kusema mtoto
wake hana njia ya uzazi, nilipomcheki nikagundua njia iko wazi na kuna kidonda
kilichotokana na kukeketwa,” anasema.
Anaongeza kuwa kati ya mwaka jana na mwaka huu amekutana na
wagonjwa watatu wenye matatizo yaliyosababishwa na kukeketwa. Anasisitiza
ukeketaji uliopo hivi sasa unafanywa katika umri mdogo.
Akizungumzia athari za ukeketaji ni kupoteza damu nyingi, pale anapokeketwa mtu kinatokea kidonda na
kutengeneza usaha ambao hupandisha homa na kuleta ufinyu wa njia ya uzazi hivyo
mama wakati wa kujifungua huchanika.
Anasisitiza katika wilaya hiyo ukeketaji upo kila mahali.
Chanzo chake ni mila na desturi kwa kuwa watu hawataki
kubadilika , pia wanasema kama msichana hajakeketwa hafai kuolewa. Hiyo ni
dhama potofu.
Anasema pamoja na elimu inayotolewa jamii bado haijakubaliana
na hiyo dhana ya kutokukeketa kutokana na mila na desturi. Hiyo ni kasumba yao
bado haijawatoka.
Anashauri elimu iendelee kutolewa kuhusu athari zake baadaye
kuhusu uzazi bora.
Pia hata mkono wa sheria unapokuwepo ufuate mkondo wake.
Mratibu wa Shirika la Afya na Maendeleo (Gesodea) pia
Mwenyekiti wa Mtandao wa Malezi, Makuzi na Maendeleo ya mtoto mdogo, Tawi la
Manyara Jackson Suloo anakiri ukeketaji
Mbulu umepungua kutokana na elimu inayoendelea kutolewa.
Pia anaamini miaka ijayo tatizo hilo litakuwa limekwisha, na
kwamba tokea mwaka jana hadi sasa taasisi yake imezungumza na wazazi 83 kuhusu
athari za ukeketaji.
Anaelezea chanzo cha ukeketaji ni kwamba ngariba wanatafuta
kipato.
Kwa upande wake WP 4728 Koplo Glory kutoka kituo cha Polisi
Mbulu anayeshughulikia dawati la jinsia anasema, kituoni hapo hakuna kesi
zozote za ukeketaji zilizofikishwa.
Wilaya ya Mbulu ni mojawapo ya wilaya zilizopo katika Mkoa wa
Manyara. Katika sensa ya mwaka 2012 idadi ya wakazi wa wilaya hiyo ilihesabiwa
kuwa 320,279 waishio humo.
Mbulu imepakana na Mkoa wa Arusha pamoja na ziwa Eyasi upande
wa kaskazini, wilaya ya Babati Vijijini upande wa mashariki, wilaya ya Hanang
upande wa kusini na mkoa wa Singida kwa magharibi.
Wenyeji asilia ni Wairaqw
ama wanajulikana kama Wambulu. Makao makuu yapo Mbulu mjini na mji huu
ulianzishwa wakati wa koloni ya Afrika ya Mashariki ya Kijerumani kwa jina la
Neu-Trier.
Ukeketaji hapa nchini badi upo katika baadhi ya maeneo kama mkoa wa Manyara, Dodoma, Arusha,
Singida, Mara, Kilimanjaro na Morogoro.
Kati ya mikoa hiyo saba, Mkoa wa Manyara ndio unaongoza kwa
asilimia 70.8 na Morogoro ndio wa mwisho kwa asilimia 21.1.
Hakuna maoni:
Chapisha Maoni