Alhamisi, 31 Desemba 2015

Ndoa za utotoni


Na Lucy Ngowi
NDOA za utotoni huathiri afya kwa kuwa mwili wa mtoto unakuwa hauko tayari kukabiliana hali hiyo, pia huleta athari za kisaikolojia.
Katika Wilaya ya Hanang, Mkoani Manyara kuna tatizo la kuwepo kwa ndoa za utotoni hali inayosababisha wasichana kupata mimba katika umri mdogo.
Inaelezwa kuwa katika wilaya hiyo ndoa za utotoni zipo lakini sio kama ilivyokuwa zamani, na kwamba watoto wanavyoolewa sio hiari yao bali hulazimishwa na wazazi wao.
Hapo zamani kwa kabila la wabarbaig msichana alikuwa haruhusiwi kuzungumza lolote kuhusu kijana anayempenda, ila wazazi ndio walikuwa wakiwatafutia wachumba.
Ama msichana anapokuwa akichunga kijana anayempenda humkamata na kuishi naye, kwa siku chache endapo msichana atarudi nyumbani kwao, wazazi wa binti huyo humrudisha kwa kijana huyo.
Mwanamke Anna Mussa (jina lisilo rasmi), anasema alipewa mimba akiwa na miaka 12, hivi sasa ana watoto watano.
Anasema akiwa katika hali hiyo  mwanzoni haikuwa rahisi kwa kuwa hakuweza kumudu maisha ya ndoa, lakini kwa kuwa mwanamme huyo aliamua kuishi naye hivi sasa wana watoto hao watano.
Kwa maelezo yake alizaliwa mwaka 1979, hivi sasa ana watoto wakubwa kabisa ambao wengine wameolewa na kuoa na wengine bado wapo shuleni.
“Kwangu mimi niliona kama nimepata bahati kwa kuwa vijana wengi wanawapa wasichana wadogo mimba kasha huwakimbia, hawako tayari kuwahudumia kwa jambo lolote lile. Huyu wa kwangu alikubali tuendelee kuishi hadi hivi leo,” anasema mwanamke huyo.
Akizungumzia hilo Ofisa Maendeleo ya Jamii wilaya ya Hanang, Sabina Sulle anasema ndoa za utotoni zinaenda sambamba na mimba za utotoni.
Watoto wengi wanaopata mimba hufika ofisini kwao kwa ajili ya kulalamikia kutopata matunzo ya watoto au mtoto aliyezaliwa.
Anasema kesi za utelekezaji wa watoto ofisini kwao zipo nyingi, ambazo hupelekwa hapo kwa ajili ya kutafuta ufumbuzi wa jinsi ya kumlea mtoto au watoto waliozaliwa.
Anasema ofisini kwao, wana kesi ya binti moja mwenye miaka 17 ambaye alipata mimba utotoni.
“Binti huyo alizaa na mume wa mtu, hivyo akawa hapati matunzo baada ya kujifungua. Kesi ilipofika kwetu tukaitatua kwa kumwamuru mwanamme huyo kumtunza mtoto hadi atakapofikia miaka 18,” anasema.
Pia ushauri mwingine wanautoa wanashauri mtoto atakapofika miaka 17 anatakiwa kuulizwa kama anataka kuishi na baba yake.
Anasema kesi nyingine walizonazo ni za kutekeleza watoto. Hizo zipo nyingi kwa kuwa wanaume wengi hawawatunzi watoto hivyo pale wanawake wanapozidiwa huenda ofisini kwao kutafuta msaada.
Pamoja na kutatua kesi nyingi, ofisa huyo anasema kuna changamoto zake kwani wanaume wengi ni waongo wanaweza kuzungumza kuwa watawatunza watoto baada ya kufikishwa hapo lakini utekelezaji unakuwa haupo.
“Hivi sasa tuna daftari mtu akija kushtakiwa anatakiwa alete hela hapa ofisini  na huyo mwanamke aifuate hapo. Mwanamme anapopeleka hela anasaini na mwanamke anapochukua pia,” anasema na kuongeza kuwa kesi hizo zinazidi 30.

Hakuna maoni:

Chapisha Maoni