Daftari laandaliwa kudhibiti utelekezaji wa familia Hanang
- Linawabana wanaume kutoa matumizi kwa watoto kwa kusaini
Na Lucy Ngowi
UKATILI wa kijinsia maana yake ni unyanyasaji wa aina yoyote
anaokutana nao mwanaume au mwanamke kwa sababu tu ya jinsia yake.
Kwa mfano shambulio la mwili kama kumpiga mwanamke. Watu wengi
kutokana na mfumo dume ulioko wanadhani kuwa kitendo hicho ni sawa kumbe sio.
Katika wilaya ya Hanang una ukatili wa aina nyingi ukiwemo wa
kutelekeza mke, watoto ama vipigo kutokana na ulevi uliokithiri kwa wanaume.
Ofisa maendeleo ya Jamii wa Wilaya ya Hanang, Sabina Sulle
anasema ukatili mkubwa wa kijinsia upo
kwenye utelekezaji wa watoto.
Anasema katika wilaya ya Hanang kesi za kutelekeza watoto zipo
nyingi kwani wanaume wengi sana wanakwepa jukumu lao. Hivyo wanawake
wanapozidiwa ndipo utafuta msaada kwao.
Anasema wanakutana na changamoto sana katika kutatua kesi za
aina hiyo kwa kuwa wanaume wengi ni waongo, wanaahidi kuwahudumia baada ya
kufikishwa kwao lakini, hawatekelezi.
Kutokana na hali hiyo imewabidi wawe na daftari ofisini ambapo
mwanamme akikubali kuhudumia watoto wake kila mwisho wa mwezi anapeleka pesa
hapo na kusaini, na mwanamke anakwenda kuchukua hapo hapo ofisini na kusaini,
jambo ambalo limesaidia sana.
Anasema kesi kama hizo kwa mwaka huu zinazidi 30.
Kwa upande wake Mratibu wa Hanang Women Conceling and
Development Association Mary Gitagno wa kata ya Ganana, anazungumzia ukatili wa
aina nyingine ni kurithiwa baada ya mume kufariki.
“Ukatili mwingine ukifiwa unarithiwa. Kwanza unatakaswa.
Wakati unaendelea kupata maumivu ya mume wako aliyefariki, anakuja mnyaturu
analeweshwa pombe usiku, mwanamke unapewa sehemu ya kulala siku hiyo unajikuta
uko mwenyewe, mnyaturu huyo anakuja kufanya tendo la ndoa na analipwa ukikubali
unakuwa umeshatakaswa,” anasema Gitagno.
Anasema wanawake wengi hawapendi hali hiyo hukataa na
kukimbia, ndio chanzo cha kupoteza mali za mume wake.
Anasema mambo mengi ya mila kama hayo hufanywa kisirisiri bila
wengine kujua.
Mama mmoja Neema Alex (jina lisilo rasmi) mwenyeji wa Kata ya
Basuti, tarafa ya Basuti, anasema mume wake alipofariki miaka mitano iliyopita,
aliletewa mtu kwa ajili ya kutakaswa.
Kwa maelezo ya mama
huyo, siku hiyo jambo ambalo sio la kawaida alijikuta akiwa amelala mwenyewe
wanawake wenzake wakiwa hawako, usiku ulipokuwa mwingi, akaja mlevi mmoja na
kutaka kumwingilia kwa nguvu, alishtuka na kukimbia.
Mtu Yule aliyeandaliwa alienda kudai ujira wake kwa
waliomwagiza, huku nyuma yeye alikuwa akitafutwa ili apigwe lakini alikimbia na
kwenda polisi.
Anasema kama jambo hilo lingefanikiwa angerithiwa na ndugu wa
mume wake.
Anasema kwa kufanya hivyo ndio maana wanawake wengi wa
vijijini wanaambukizwa magonjwa mbalimbali.
Daktari wa Kituo cha Afya cha Katesh, David Laizer anasema
ndoa za utotoni zinazosababishwa na wazazi ni ukatili mkubwa, kwa kuwa kitendo
hicho si kwa ridhaa ya muolewaji.
Pia anasema ukatili mwingine anaouana ni ule wa kuwapeleka
watoto wa kiume shuleni na kuwaacha wa kike. Huo ni ukatili uliopitiliza kwa
jamii hiyo.
Pia wanaume kutelekeza wake zao na watoto ni ukatili mkubwa
kwa kuwa watoto wale wanateseka kwa kukosa mahitaji muhimu.
Wengi wanatelekezwa ama kuachika wanakuwa hawana sehemu za
kwenda hali inayoleta mateso kwa watoto.
Kwa upande wake Mtendaji wa Katesh, Peter Mando anasema katika
eneo hilo ukatili wa kijinsia upo sana kwa wanaume kuwapiga wake zao pamoja na
kuwafukuza nyumbani.
“Migogoro kama hii tunaisuluhisha sana sisi na maofisa wa
jamii, mahakama na polisi. Bado changamoto hiyo ni kubwa sana,” anasema.
Anasema katika kutatua migogoro hiyo wanawatumia maofisa wa
maendeleo ya jamii kusuluhisha ikiwa ni pamoja na wazee wa mila na mahakama.
Chanzo cha jambo hili anasema ni mila na desturi za huko kwani
wanaume wamekuwa wakiwabeza sana wanawake, ugumu wa maisha kwani wanandoa wengi
wamekuwa wakizozana kwa ajili ya mahitaji ya nyumbani.
Si hivyo tu, bali na unywaji wa pombe pamoja na kutokufanya
kazi, ndiyo inaleta shida hii.
Mwalimu Mkuu wa shule ya msingi Katesh A, Petro Tehhan anasema
ukatili wa kijinsia eneo hilo unasababishwa
na mfumo dume pale baba anataka kusema kila kitu.
Pia kutokuelewana kwa mume na mke kunasababisha hali hiyo.
Mkuu wa Polisi wa wilaya ya Hanang Kituo cha Katesh, Hamis
Mwampelwa anazungumzia kesi za ukatili wa kijinsia zilizoripotiwa kituoni hapo
ni 161, kati ya mwaka 2014 hadi sasa.
Anasema katika kesi hizo zile zilizofungwa ambazo
hazikufikishwa mahakamani ni kesi 38, zilizofikishwa mahakamani ni 59 na zilizo
chini ya upelelezi ni 70.
Kati ya kesi hizo, Mwampelwa anasema zilizopata mafanikio ni
15, ambazo hazikupata mafanikio ni 14, kesi iliyopo mahakamani kwa mwaka huu ni
moja.
Anaeleza miongoni mwa kesi zilizoripotiwa za unyanyasaji wa
kijinsia kuwa ni zile za kutelekeza familia, kubaka, shambulio la aibu pamoja
na ukatili dhidi ya mtoto.
Anatoa mfano kwa kesi moja iliyofikishwa kituoni hapo siku za
karibuni.
Kesi hiyo inamhusu mkazi wa Kitongoji cha Qedang’onyi Emanuel
Lambo (50), aliyetarajiwa kufikishwa mahakamani baada ya kumtendea vitendo vya
ukatili mtoto wake wa miaka tisa wa shule ya msingi kwa kumchoma na kisu chenye
moto mkali maeneo mbalimbali ya mwili.
Mwampelwa anasema mtoto huyo alichomwa moto maeneo mbalimbali
ya mwili, kwenye kiwiko mkono wa kulia,
kwenye shavu kushoto, shingoni kushoto, usoni na sehemu mbalimbali za mguu
upande wa kulia kutokana na kulala kwa kaka yake, Mussa Emmanuel.
Anasema Oktoba 15 sueta la shule la mtoto huyo lilikuwa
halijakauka, mama yake akamwagiza kaka yake akamuombee ruhusa shuleni, kisha
mtoto huyo akalala kwa kaka yake huyo ndio ilikuwa chanzo cha baba kutenda
ukatili huo.
Anasema mwanafunzi huyo aliwaambia wakati akitendewa ukatili
huo, mama yake alijitahidi kumwokoa lakini baba yake alimkataza.
Tukio hilo la mwanafunzi kutendewa ukatili, lilijulikana baada
ya mwalimu wake Bahati Mwiru kuhakiki wanafunzi shuleni na kugundua mtoto huyo
hayuko, ndipo wenzake wakamwambia ana majeraha.
“Mwalimu aliendelea kuuliza wanafunzi hao majeraha ni ya nini, ndipo wakamwabia amechomwa moto
na kisu. Wakaijulisha kamati ya shule, mwenyekiti na mlinzi wakaenda kumchukua
nyumbani,” anasema.
Anasema mwalimu huyo alitoa taarifa polisi baada ya mtoto huyo
kukosekana shuleni kwa muda na alipouliza wenzake walimwambia anatibu majeraha
aliyosababishwana baba yake, ndipo wakaanza kumfuatilia.
mwisho
Hakuna maoni:
Chapisha Maoni