Na Lucy Ngowi
ELIMU ya mahitaji maalumu hutolewa kwa watoto wenye matatizo
ya kujifunza ili kuwawezesha kupata huduma za elimu.
Watoto hao ni wale walio na ulemavu wa kutokuona, viziwi,
ulemavu wa akili, ulemavu wa usonji, viziwi wasioona, ulemavu wa viungo na
walemavu wa ngozi.
Wenye mahitaji haya hutakiwa kupewa upendo wa hali ya juu
kutoka kwa wazazi, familia, walezi, jamii inayowazunguka na wanafunzi wenzao
shuleni ili nao wajione kuwa wanastahili kuwepo duniani.
Lakini kinyume cha hapo, huwaongezea maumivu na mateso watoto
hao, kwani kwa kutokuwapa elimu stahiki hilo ni tatizo ama kwa kutokupewa
huduma bora za chakula, malazi na mavazi.
Jamii inapotoa mapenzi ya kweli kwa watoto hawa hujisikia
furaha sana. Sasa basi ni vema jamii kuzidisha mapenzi ya dhati kwa watoto hawa
pamoja na serikali.
Mchango wa serikali nao unahitajika kwa kiasi kikubwa ili
kuwafanya watoto hawa wasiwe wapweke. Inatakiwa serikali itoe huduma zote
stahiki kwa watoto hawa ili waweze kusoma kwa bidii na hatimaye watakapomaliza
wapate nafasi nzuri kikazi.
Kwa upande wake Wizara ya Elimu na Mafunzo ya Ufundi
inajitahidi kuwa na shule pamoja na vitengo mbalimbali kwa ajili ya watoto hao
wenye mahitaji maalum, lakini zimekuwa
zikikabiliwa na changamoto mbalimbali zikiwemo za fedha na vifaa maalum kwa
ajili ya kufundishia.
Nimeanza kueleza hayo baada ya kupata nafasi ya kutembelea
Shule ya Msingi ya Katesh A, iliyopo wilaya ya Hanang mkoa wa Manyara.
Shule hiyo pia ni ya bweni kwa ajili ya kuwasaidia watoto
wanaoishi katika mazingira magumu ikiwemo wale wenye mahitaji maalum.
Katika shule hiyo ya Katesh A pia ni ya mchanganyiko kwa maana
kwamba inachukua watoto wenye mahitaji maalum, mazingira magumu na watoto wa
kawaida.
Wenye mahitaji maalum ni kama hao niliowaeleza hapo juu na
waliotoka kwenye mazingira magumu ambayo wazazi wao wamekuwa wakihama hama na
mifugo, kutokuelewana na maisha duni ya familia husika wapo 106.
Mwalimu Mkuu wa shule hiyo Petro Tahhan anasema viziwi shuleni
hapo wanasoma madarasa tofauti, wasioona wanachanganywa darasa la tatu na wale wengine wasio na matatizo na wale wa
mtindio wa ubongo hufundishwa na walimu maalum.
Anaelezea changamoto za wasioona kuwa wana upungufu wa vifaa
vya kufundishia kama mashine za Braille. Mashine hizo zipo chache kwani
ilitakiwa kila mwanafunzi asiyeona awe na yake.
Tahhan anasema wanafunzi hao wasioona wapo nane, wavulana watano na wasichana watatu.
Darasa la awali yupo mmoja, la kwanza yupo mmoja, la pili wapo
wawili, la tatu wapo wawili na la tano wapo wawili.
“Mashine nzima ni mbili walimu ambazo walimu wanatumia lakini
kiuhalisia ilipaswa kila mwanafunzi awe na ya kwake. Kunatakiwa kuwe na walimu
15. Katika shule hii pia tuna walimu wasioona wawili ambao wanafundisha
madarasa ya kawaida,” anasema mwalimu huyo.
Anasema wanafunzi hao wasioona hawana vitabu vya kuwafundishia
kwa maana kuwa hawana vitabu vyao vinavyowahusu bali wanatumia vya kawaida.
Anasema miundombinu shuleni hapo sio rafiki kwani wanatakiwa
kuwa na mazingira rafiki na vyoo vyao wenyewe.
Pia wana upungufu wa vifaa vya michezo, hata viwanja vyao vya
kuchezea hakuna.
changamoto nyingine kwao ni suala la maji shuleni hapo ni
tatizo, hivyo inabidi wazoee mazingira hayo, mara nyingine wanachota wenyewe
ama wenzao wanawasaidia.
Na pia ulinzi ni shida shuleni hapo hakuna uzio.
Akizungumzia wanafunzi viziwi shuleni hapo anasema wapo 27 ambao wanatakiwa kusoma miaka
10 badala ya saba ya kawaida. Darasa la kwanza, la tatu na la tano wanasoma
miaka miwili miwili.
Wanasoma kwa mfumo huo kwa kuwa wanakuwa wanachelewa kuelewa
kile mwalimu anachofundisha, ila madarasa mengine wanasoma mwaka mmoja mmoja.
Anasema shule hiyo ina upungufu wa vyumba vya madarasa hivyo
wakati mwingine wanachanganywa wote katika chumba kimoja, pia wana tatizo la
walimu wenye uwezo wa kufundisha watoto hao wenye mahitaji maalum.
Jambo lingine ni kwamba mihtasari wanayotumia ni ya kawaida
haiendani na mahitaji yao.
Tatizo lingine ni kwamba hawana kamusi yao ya lugha ya alama.
Analitaja kundi lingine ni la albino ambao hivi sasa wapo
nane, awali walikuwa 11 lakini watatu wamemaliza. Wanafunzi hao wanakabiliwa na
tatizo la vifaa vya kujikingia ngozi yao kama mafuta yao na kofia.
Mwalimu mkuu huyo anasema wale wa utindio wa ubongo wapo
watano, kati ya hao wawili ni wa kiume na watatu wasichana.
“Hawa wa utindio wa ubongo kwa sasa wapo nje ya shule. Wana
upungufu wa walimu, mihtasari yao hakuna, hivyo kwa sasa wanapelekwa na wazazi
wao shuleni hapo,” anasema mwalimu huyo na kuongeza kuwa kitengo hicho cha
utindio wa ubongo kimeanza mwaka huu.
Kwa wanafunzi hao wa utindio wa ubongo, wanafundishwa na
mwalimu wa kiume lakini walitakiwa walimu wa kike pia kwa sababu wanahitaji
huduma za ziada kama kusaidiwa kwenda chooni ama kulishwa ama wakati mwingine
kuvalishwa nguo kama wamejichafua.
Anasema kuwa shule hiyo haina mipaka wanaweza kwenda kutoka
mikoa yote nchini, kwani mbali na wakutoka wilaya hiyo wengine wanatoka Tanga,
Simanjiro, Singida, Babati na Mbulu.
Tahhan anashauri shule hiyo ingeangaliwa kwa jicho la kipekee
kwa kuwa ni shule ya mahitaji maalum, kwani fedha wanazopewa ni kwa ajili ya
chakula tu, hakuna ya kumlipa mlezi wala vinginevyo.
Kwa upande mwingine Mwalimu Mkuu msaidizi Caroline Lema
anasema kama serikali imeamua kutenga shule hiyo hapo Hanang iwasaidie watoto
kwa kuwapa vifaa vyao stahili ili ule umaalum uonekane.
“Watoto hawa inatakiwa watibiwe walau kwa mwaka mara mbili,
kama ni wasioona inabidi wachunguzwe wote uoni wao lakini kwa pesa inayotolewa
inatosheleza kwa chakula tu, sasa hii ni elimu maalum kwa vipi? kama hata hela
ya matibabu hakuna?,” anahoji Lema.
Mwalimu huyo anasema kuna watoto watatu ambao wanatakiwa
waende katika hospitali ya KCMC Kilimanjaro kwa ajili ya kufanyiwa upasuaji
haraka iwezekanavyo lakini kwa kuwa hakuna fedha hawajaenda.
Anasema kila halmashauri yenye elimu maalum huwa anakuwepo
ofisa elimu maalum lakini anakuwa na fani moja labda ya viziwi sio utindio wa
ubongo, lakini anafikiri ilibidi kuwe na maofisa mchanganyiko ama huyo ofisa
asiwe amejikita kwenye eneo moja tu.
Kwa upande wake mwalimu Anna Mark anayefundisha wanafunzi
wasioona shuleni hapo anasema changamoto kubwa ni ukosefu wa vifaa vya
ufundishaji.
“Vifaa vingi tunaweza kuvitengeneza wenyewe ambavyo
vinawasaidia watoto hawa,” anasema mwalimu huyo na kuongeza kuwa upungufu wa
mashine za Braille ni changamoto kwake na wanafunzi hao.
Akiwaelezea watoto hao jinsi wanavyopokea kile
anachowafundisha anasema wanajitahidi kupokea vizuri japo kwa taratibu sana.
Mwanafunzi wa darasa la pili Imani Agustine anasema anapata
ugumu pale anapoandikiwa neno jipya hata kama amefundishwa anashindwa kulisoma.
Naye Paulo Marcelly anasema somo la hisabati linampa shida
hivyo anaiomba serikali kuwapatia vitabu na mashine.
Naye Ofisa Elimu Maalum wa Hanang, Albart Machua anasema
katika shule ya Katesh A kuna changamoto nyingi sana ikiwemo vyumba vya madarasa na vifaa vya kufundisha na
kujifunzia.
Anasema kuhusu fedha za matibabu za wanafunzi hao hutolewa na
halmashauri, japo kuna baadhi ya wanafunzi walihitajika kwenda KCMC kufanyiwa
upasuaji wa macho, hawakwenda kwa kukosa pesa.
Pia anaomba serikali ijitahidi kufikisha hela za ruzuku kwa
wakati ili wanafunzi hao waweze kuhudumiwa.
Kwa upande wake Ofisa elimu wa wilaya ya Hanang, upande wa
shule ya msingi, Gwandu Omari anasema wanafunzi hao wanatakiwa watengwe
kutokana na ulemavu walionao.
“Katika shule ya Katesh A kuna changamoto ya mabweni yaliyopo
hayatoshi, ni chakavu, magodoro machache, jiko na bwalo vyote vina upungufu,”
anasema.
Pia anasema baadhi ya fani zinazohusu watoto wenye mahitaji
hayo kuna upungufu wa walimu, wapo watano ila mahitaji ni 13.
Hata mashine za watoto wenye shida ya macho ni chakavu
zinafanyiwa matengenezo kila wakati, karatasi zake ni za shida.
Viziwi wanatakiwa wawe na mashine na tochi za kuwakagua hali
zao za masiko kila wakati lakini hakuna.
Albino nao ni shida huduma zao, wanahitaji kuchekiwa ngozi zao
mara kwa mara. Kuna gharama za kila wakati kliniki na kupewa mafuta maalum.
“Hawa wa mtindio wa ubongo huduma zao ni za karibu sana popote
anahitaji msaidizi, inapokuwa ni mwalimu peke yake kazi inakuwa kubwa,”
anasema.
Akizungumzia miundombinu bado kuna tatizo kubwa hakuna ufumbuzi wa haraka wa kuongeza
madarasa na mabweni yaliyopo ni chakavu yanatakiwa kubomolewa.
Kwa upande wake Mratibu wa Elimu Maalum kutoka wizara ya
elimu, Gryson Mlanga anataja idadi za shule maalum na vitengo katika maeneo
mbalimbali nchini.
Mlanga anasema idadi za shule kwa wasioona zipo nne Tanzania
nzima ambazo ni Irente Lushoto, Buigiri Chamwino, Malangali Sumbawanga na
Furaha Tabora.
“Hizi ni shule maalum. Uoni hafifu na albino na wasioona
kabisa,” anasema.
Kwa upande wa shule mchanganyiko zipo 34, ambapo katika shule
hizo darasa la kwanza na la pili wanakuwa na madarasa maalum, kuanzia la tatu
mpaka la saba wanachanganyika na wasiokuwa na ulemavu.
“Hizi shule zina mabweni. Nazo ni uhuru mchanganyiko iliyoko
Dar es Salaam, Pongwe Tanga, Same Kilimanjaro, Mwereni Moshi, Longido, Katesh A
wilayani Hanang, Ikungi Singida na Hombolo mkoani Dodoma,” anasema.
Mratibu huyo anasema
kwa viziwi shule maalum zipo 11 na vitengo 37. Vitengo ni vile vinakuwepo
kwenye shule za kawaida ambapo hutengwa madarasa maalum.
Anataja baadhi ya shule hizo za viziwi kuwa ni Buguruni,
Mwanga, Njombe, Tabora viziwi, Twivila Iringa na Tumaini Singida.
Baadhi ya vitengo kwa viziwi ni Mugeza huko Bukoba, Msasani
Dar es Salaam, Maweni Kigamboni, Twiga eneo la Temeke na Basil Mramba huko
Mwanga, Kilimanjaro.
Kwa upande wa ulemavu wa akili zipo shule tano maalum ambazo
ni Sinza maalum, Mtoni Maalum, Miyuji Dodoma, Bethlehemu Ifakara na Lulindi
huko Masasi.
Ina zaidi ya vitengo 250 ambavyo ni Leganga Arusha, Rutihinda
Kinondoni, Umoja Kinondoni na Msasani zote zikiwa mkoa wa Dar es Salam.
Ulemavu mwingine ni ule wa usonji ambapo watu hao wameathirika
katika mishipa ya fahamu, unaathiri mahusiano, ufahamu na mawasiliano.
Katika huo kuna vitengo vitano kwa Dar es Salaam na Morogoro.
Vipo Msimbazi Mseto, Patandi na Uhuru Arusha, Kiwanja cha ndege Morogoro na
Mbuyuni.
Wengine ni wanafunzi wasioona amboa wako kwenye vitengo. Uhuru
mchanganyiko, Mwanga, Mugeza Bukoba, Makalala Mufindi na Katumba Two, Tukuyu.
Akizungumzia wenye mahitaji maalum ya ulemavu wa viungo husoma
kwenye shule za kawaida kama hawana shida kubwa.
Hao wenye ulemavu wa viungo wengine huwepo Jesho la Wokovu
jijini Dar es Salaam, Faraja mkoani Kilimanjaro, Malangali, Kabanga Kasulu
mkoani Kigoma huko nako wapo wasioona na albino. Na Siuyu mkoani Singida.
Mratibu huyo anasema changamoto zipo na wanazipata kwenye
taarifa mbalimbali zinazowafikia, pia wanapopata fursa za kutembelea shule hizo
hukutana nazo.
Akielezea mahitaji wanayopaswa kupewa wanafunzi hawa kutoka
serikalini ni chakula, malazi safi, matibabu, nauli wakati wa likizo, vifaa vya
kufundishia na vya kujifunzia kulingana na mahitaji husika.
“Kama wizara tunatarajiwa watoto hawa wahudumiwe katika maeneo
hayo,” anasema.
Kuhusu vifaa vya watoto hao, anasema kwa muda mrefu
vilinunuliwa na wizara, lakini ikafika mahali ikaamuliwa vitolewe na
halmashauri na sasa hivi kuna mradi unaotekelezwa nchi nzima wa kuvinunua.
“Zitanunuliwa mashine 800 za Braille, shime sikio 1000, fimbo
nyeupe 1200 pia tunaendelea kuchapisha vitabu 8000 ambavyo vitasambazwa vya
mtaala mpya,” anasema na kuongeza kuwa vifaa hivyo vitatolewa kabla ya mwaka
huu haujaisha.
Anasema suala la walimu ni jukumu la Ofisi ya Waziri Mkuu –
Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa (TAMISEMI).
Anasema mpango wa baadaye ni kwamba kila halmashauri iwenna
shule moja maalum kwa ajili ya wanafunzi wa mahitaji maalum.
Anasema takwimu sahihi za wanafunzi hao hazipo ila kuanzia
sasa zinaanza kukusanywa mpaka mwaka 2020 zitakuwa zipo tayari.
mwisho